|
|
|
|
|
|
|
|
VICENT MBILINYI Bondia anayetamani mafanikio
VICENT Mbilinyi miongoni mwa mabondia wanaoanza kufanya vizuri katika medani ya masumbwi huku ndoto yake ikiwa ni kufanya vema kitaifa na kimataifa ili kujiweka katika ramani nzuri ya mchezo huo Afrika na Dunia. Nyota huyo kwa sasa ananolewa na kocha wa kimataifa wa mchezo huo hapa nchini, Rajabu Mhamila maarufu kwa jina la Super D ambaye anasifika kwa kukuza na kuviendeleza vipaji vya mabondia wachanga hadi kufikia mafanikio. Wapo mabondia wengi ambao kwa sasa wanaonekana kupiga hatua nzuri katika mchezo wakiwa chini ya Super D akiwemo Mbilinyi ambaye hadi sasa ameshapigana mapambano tisa huku akipoteza moja na kushinda matano akitoa sare mawili na kupoteza pambano moja. Licha ya kutofanya vema katika kupata ushindi, mapambano mengi ambayo amepigana ni moja ya njia sahihi ya kupiga hatua nzuri katika mchezo ambayo kila bondia anatamani kufikia. Akiwa katika mchakato wa kufikia mafanikio, Mbilinyi anavutiwa vema na bondia anayefanya vizuri ulingoni Thomas Mashali 'Simba Asiyefugika' ambaye kwa sasa anajiandaa na pambano lake dhidi ya Francis Miyeyusho Desemba 25, mwaka huu mkoani Morogoro. Mbilinyi anakiri kuwa sababu ya kuvutiwa na Mashali ni namna anapokuwa kwenye mawindo ulingoni kwa maana anatumia akili nyingi katika kushambulia na ni mwepesi wa kurusha makonde na kurudi haraka kwenye eneo lake. "Napenda Mashali anavyokuwa ulingoni na napenda kuwa kama yeye na ndiyo maana nafanya mazoezi kwa nguvu nikiwa chini ya Super D na ninaamini ndoto yangu ya muda mrefu itatimia ya kuwa bingwa Afrika na Dunia. "Ninachoomba tu mapromota wanitafutie mapambano ya kimataifa ili nioneshe uwezo wangu kwa maana nia ninayo kinachohitajika ni kupewa fursa niitumie kuonesha kipaji changu nilichojaaliwa na Mungu, Muumba Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo," anasema. Nyota huyo ambaye ni mtoto wa nne katika saba wa Mzee Alphonce Mbilinyi ambaye ametangulia mbele ya haki anasema kuingia kwake katika mchezo huo ni sehemu ya ndoto yake tangu akiwa Shule ya Msingi Mzimuni iliyopo Magomeni, Dar es Salaam. Mbilinyi anasema licha ya kuingia katika mchezo pia ni mchezaji mzuri wa mpira wa miguu anafiti vema akicheza namba tano na Yanga ya Dar es Salaam ndiyo timu anayoishabikia na kimataifa anaihusudu Chelsea ya Uingereza. Bangi Nyota huyo anasema hajawahi kutumia kilevi hicho kama ilivyo kwa baadhi ya mabondia na kufafanua hafikirii kukitumia kwa maana ni moja ya kilevi kinachoharibu mwili na mwelekeo hususan kwa mabondia. "Sifikirii kutumia kwa maana naona namna inavyowaathiri baadhi ya mabondia wanaotumia bangi kwani wakati mwingine wamekuwa wakifanya vitendo viovu ndani au nje ya ulingo na kusababisha kuharibu taswira nzima ya masumbwi na kufanya jamii kuutafsiri vibaya kumbe si wote tuko hivyo," anasema.
Anafafanua kuwa baadhi ya mabondia wanaamini kuwa bangi ni moja ya chachu ya ushindi katika mchezo kitu ambacho si kweli, kinachotakiwa ni kufanya mazoezi ya kutosha na kutumia mbinu za mchezo ili kufanikisha ushindi. Ushirikiana Nyota huyo ambaye Desemba 25 mwaka huu anapanda ulingoni kuzipiga na Deo Njiku katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro anasema kuwa haamini kama ndumba zinasaidia kushinda pambano. "Hizo ni imani potofu ambazo hazina msingi katika mchezo wa masumbwi kinachotakiwa ni kujiamini unapokuwa ulingoni kwa kumsoma mpinzani wako na zaidi ni kufanya mazoezi ambayo ndiyo yanayokuhakikishia ushindi na si tofauti na hivyo," anasema. Nje ya ndondi Bondia huyo wa Kibaha mkoani Pwani anasema kuwa nje ya mchezo huo anashughulika na biashara ndogo ndogo ambazo zinasaidia kumweka vizuri katika tasnia ya masumbwi nchini. Anasema kuwa kama si kuwa na biashara maisha yake yangekuwa na changamoto nyingi katika kuyaendesha kwa maana bado hajapata mafanikio ya kuridhisha kupitia masumbwi na kusababisha kutumia kipato chake kukiiingiza kwenye masumbwi. Kwani mara kadhaa hutumia kipato chake anachokipata kupitia biashara kununulia baadhi ya vifaa vya ndondi ambavyo vimekuwa ni changamoto kubwa kwa mabondia wanaoanza kupata majina kupitia mchezo huo. Hivyo anatoa mwito kwa mabondia wanaochipukia kuwa na shughuli tofauti ili kufanikisha kufanya mchezo huo kwa umakini na kusaidia kuondoa changamoto nyingi zinazohitaji kusukuma maendeleo ya masumbwi. Bondia huyo anayepigania uzito wa kilo 63 pia anatoa mwito kwa mabondia wenye majina makubwa ambao wanapata nafasi ya kucheza mapambano ya kimataifa kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kutosubiri safari. Anafafanua kuwa jambo hilo litasaidia kupata ushindi katika michezo wanayopata kimataifa na kutoa njia kwa wengine kupata nafasi za kwenda nje ya nchi katika mapambano.
|
|