Anko Hashim Lundenga enzi za uhai wake.
Na Kionambali M.Kionambali
Kisiju/Mkuranga
S.L.P 2785
____________________
NI msiba mzito kwa familia ya urembo Tanzania.
Rafiki yetu Hashim Lundenga' Anko Hashim ambaye ni muasisi wa shindano la urembo 'Miss Tanzania' ametangulia mbele ya haki.
Anko Hashimu mwendo ameumaliza Aprili 19 mwaka huu Jijini Dar es Salaam baada kuugua kwa muda mrefu.
Huyu ndiye mwamba aliyeitambulisha Tanzania duniani kupitia shindano hilo.
Alifanya kazi kubwa ya kubuni wazo la kuanzisha shindano hilo na kisha akalitekeleza kwa vitendo.
Aliiongoza Kamati ya Miss Tanzania kupita kila pembe ya nchi kusaka wasichana warembo.
Haikuwa kazi nyepesi kwani ikumbukwe zama hizo dhana iliyokuwepo shindano hilo lilionekana ni uhuni.
Walifanya kazi mbili kubwa.Kwanza kutoa elimu ya kuwa shindano hilo ni fursa ya kiuchumi kwa warembo.
Na haikuwa uhuni kama ilivyokuwa inaelezwa na baadhi ya watu katika jamii.
Pili walifanya ushawishi wasichana wajitokeze katika ngazi ya vitongoji waoneshe urembo waliojaaliwa na vipaji vyao ili wajifungulie fursa za kupata mikataba ya matangazo kutoka kwa makampuni mbalimbali.
Hatimaye ndoto ikatimia na shindano hilo likawa alama ya utambulisho wa Tanzania kupitia shindano la 'Miss World'.
Maelfu ya warembo wakazalishwa kila kona na wakawa mastaa kweli kweli.
Kuwataja hapa orodha ni ndefu.Haiwezekani.
Shindano likavuma kila pembe ya nchi kuliko hata mchezo pendwa wa soka.
Baada ya miaka kadhaa ya mafanikio Anko Hashim akafanyiwa zengwe na kuondolewa Kamati ya Miss Tanzania kihuni.
Huo ukawa mwanzo wa shindano hilo kupoteza mvuto na kufa rasmi.
Pumzika kwa amani Anko Hashim alama ya uasisi wako haitafutika.
Twendeni tukamzike Anko Hashim pembeni ya shindano la Miss Tanzania ili wawili hao wabaki wakipiga stori na kukumbushana nyakati zao bora walipokuwa duniani.